“Hoja
zinazoonyesha ya kwamba shirika hili ni
la uongo.”
Shirika la Mashahidi wa Yehova linajidai
kuwa hilo ndilo kanisa la kweli la pekee
hapa duniani. Linasema ya kwamba
makanisa mengine yawe ya Katoliki au ya
Kiprotestanti yote yanafunza makosa na
ya kwamba yeyote ambaye si shahidi wa
Yehova atauawa na Mungu. Hapa kuna
sababu nne ambazo zinaonyesha ni kwa
nini shirika hili linafaa kuepukwa.
1. MASHAHIDI WA
YEHOVA WANAPINGA MAFUNZO MAKUU YA BIBLIA
Mashahidi wa Yehova wanapinga kuwa
Yesu Kristo ni Mungu. Bali wanafunza
kuwa Yesu Kristo ni malaika aliyeumbwa.
Lakini Biblia inafunza wazi wazi kwamba,
Yesu Kristo ambaye ni Mwana ni Mungu.
Kwa mfano Waebrania 1:8 inasema, “Lakini
kwa Mwana anasema ‘kiti chako cha enzi,
e Mungu, ni cha milele na milele…’ ”
Vifungu vingi pia vinafunza hivi -
Yohana 1:1,14; 20:26-28; Matendo ya
Mitume 20:28, Warumi 9:5, Waebrania 1:3,
8-9; 2 Petero 1:1.
Mashahidi wa Yehova wanapinga
kufufuka kimwili kwa Yesu Kristo.
Bali wanafunza ya kwamba mwili wa Yesu
uliyeyuka ukawa mvuke. Charles Taze
Russell, mwanzilishi wa shirika hili
alifunza, “yule mtu Yesu alikufa na
amekufa milele.” (Studies in the
Scriptures Vol. 5, 1899, uk. 454).
Lakini Biblia inafunza wazi wazi kwamba
mwili wa Yesu ulifufuliwa: Kwa mfano
Luka 24:39 - “Tazameni mikono yangu na
miguu yangu. Ni mimi mwenyewe! Niguzeni
na muone; roho haina mwili na mifupa
kama mnavyoona nikiwa nayo.” Angalia pia
Yohana 2:19-21, 20:26-28; 1 Wakorintho
15:6,14.
Mashahidi wa Yehova wanapinga kwamba
Roho Mtakatifu ni Mungu. Bali
wanafunza kuwa Roho Mtakatifu ni nguvu
tu zisizo za kibinadamu kama ile ya
umeme.
Lakini Biblia inafunza wazi wazi kwamba
Roho Mtakatifu ni Mungu; Matendo ya
Mitume 5:3-4 ‘Kisha Petero akasema,
Anania, kwa nini umejazwa na Shetani
moyoni mpaka ukamdanganya Mungu Roho
Mtakatifu… hujawadanganya watu ila
umemdanganya Mungu. Angalia pia Yohana
14:16-17, 16:13-15 Warumi 8:26-27; 2
Wakorintho 3:6,17-18; Waefeso 4:30.
Mashashidi wa Yehova wanapinga wokovu
kuwa zawadi ya bure ya Mungu. Bali
wanafunza ya kuwa wokovu lazima utafutwe
kwa bidii na binadamu. Kuupata wokovu na
kuepuka hukumu, mtu lazima ajiunge na
shirika la Mashahidi wa Yehova na
vilevile afanye mambo kadhaa
linayoyaagiza.
Lakini Bibilia inafunza wazi wazi kwamba
wokovu hauwezi kupatikana baada ya
kufanya chochote - kwani hii ni zawadi
ya bure ya Mungu. Waefeso 2:8-9 –
“Tumeokolewa kwa sababu ya neema yake
kupitia kwa imani - na hii si kwa sababu
yenu bali ni zawadi ya Mungu – sio kwa
matendo yetu, ili yeyote asiringe.”
Angalia pia Warumi 4:1-4, Wagalatia
2:16, Tito 3:5.
Mashahidi wa Yehova wanapinga adhabu
ya milele ya wenye dhambi. Bali
wanafunza kwamba wenye dhambi
wataangamizwa kabisa na hawataishi tena.
Lakini Biblia inafunza kuwa kutakuwa na
adhabu ya milele ya wenye dhambi, Matayo
25:41,46. “Kisha atawaambia wale walio
mkono wake wa kushoto, niondokeeni hapa,
enyi mliolaaniwa, kwenda kwa moto wa
milele uliotengenezewa Shetani na
malaika wake... Basi wataondoka kwenda
kwa hukumu ya milele, lakini
waliotakaswa waende kwa uzima wa
milele.” Angalia pia Matayo 18:8, 2
Wathesalonike 1:8-9, Ufunuo 14:10,11;
20:10,15.
Mashahidi wa Yehova wanapinga kuwa
roho wa binadamu huishi baada ya kifo.
Bali wanafunza kuwa, kama wanyama,
maisha ya binadamu huishia kwa kifo.
Lakini biblia inafunza wazi wazi kuwa
roho wa binadamu huendelea kuishi baada
ya kifo: 2 Wakorintho 5:8 – “Tuna
uhakika, nasema, na tungependelea kuwa
mbali na mwili tuwe nyumbani na Bwana.”
Tazama pia Luka 16:19-31; Wafilipi
1:23-24; Ufunuo 6:9-11.
Mashahidi wa Yehova wanafunza kuwa
maisha ya milele pamoja na Mungu ni kwa
wachache tu. Wanadai ya kwamba
kikundi maalum cha watu 144,000 kati ya
Mashahidi wa Yehova wanaweza kuokolewa
na kuishi milele na Mungu mbinguni; hao
wengine wataishi hapa duniani.
Lakini Biblia inafunza wazi wazi kuwa
wale wote wanaoweka imani yao kwa Yesu
Kristo watapata uzima wa milele pamoja
na Mungu. Biblia inawataja watu hawa
kuwa wengi wasiohesabika: Ufunuo 7:9, 15
– “Baada ya haya nikaangalia na mbele
yangu kulikuwa na watu wengi wasioweza
kuhesabika kutoka kila nchi, kabila,
watu na lugha, walikuwa wamesimama mbele
ya kiti cha enzi na mbele ya
mwanakondoo… wako mbele ya kiti cha enzi
cha Mungu na wanamtumikia usiku na
mchana hekaluni mwake.” Tazama pia
Yohana 3:15, 5:24, 12:26; Waefeso 2:19,
Wafilipi 3:20, Wakolosai 3:1, Waebrania
3:1, 12:22; 2 Petero 1:10,11.
Mashahidi wa Yehova wanapinga Utatu wa
Mungu, na wanafunza kuwa Shetani alizua
mafunzo ya Utatu. Hivyo basi
wanatupilia mbali maandiko yoyote
yanayomtambua Yesu Kristo kama Mungu na
Roho Mtakatifu kama Mungu.
Lakini Biblia inafunza wazi wazi ya
kwamba Mwana, Roho Mtakatifu na Baba
wote ni Mungu (Yohana 1:1; 20:28,
1Yohana 5:20; Matendo 5:3, 4). Pia
inafunza na kuhimiza kwamba kuna Mungu
mmoja tu (Isaya 43:10; 44:6,8 n.k.)
Inafunza kuwa hao watatu yaani Bwana,
Mwana na Roho Mtakatifu ni Mungu mmoja.
(Matayo 28:19; 1 Wakorintho 12:4-6; 2
Wakorintho 13:14; 1 Petero 1:2).
Je, si ni hatari sana kufuata
shirika linalopinga mafunzo makuu ya
Biblia?
2. MASHAHIDI WA YEHOVA WANACHEZEA
HILA BIBLIA
Shirika la Mashahidi wa Yehova
limechapisha Biblia yao wenyewe isiyo ya
kweli. Biblia hii inaitwa Tafsiri ya
Dunia Mpya (New World Translation).
Biblia hii imejaa na mabadiliko ya
vifungu vingi vya maandiko matakatifu.
Mabadiliko haya yanajaribu kuficha
mafunzo ya Mashahidi wa Yehova ambayo ni
ya uongo na hayatokani na Biblia.
|
Ufananisho wa
Biblia na ile danganyifu ya Tafsiri ya Dunia Mpya |
|
| Biblia Takatifu |
Biblia danganyifu ya Tafsiri ya Dunia Mpya |
|
Yohana 1:1 — “Hapo mwanzo alikuweko Neno, naye Neno
alikuwako kwa Mungu naye Neno alikuwa Mungu.” Hili ni dhihirisho kuwa Yesu (Neno) ni Mungu. |
Yohana 1:1 — “Hapo mwanzo Neno alikuwako, naye Neno
alikuwa pamoja na Mungu, na Neno alikuwa mungu. Badilisho hili lilifanywa kuunga mkono pingamizi la Mashahidi wa Yehova kuwa Yesu ni Mungu. |
|
Wakolosai 1:16 — “Kwa kuwa katika yeye (Yesu) vitu
vyote viliumbwa… vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa
ajili yake.” Haya yanafunza kuwa Yesu ni muumba wa vyote, na yeye mwenyewe sio kiumbe. |
Wakolosai 1:16 — “Kwa sababu kwa njia yake vitu
vingine vyote viliumbwa… Vitu vingine vyote
vimeumbwa kupitia yeye na kwa ajili yake. Neno “vingine” limeongezwa kimakosa ili kuunga mkono mafunzo potovu ya Mashahidi wa Yehova kuwa Yesu mwenyewe ni malaika aliyeumbwa. |
|
Waebrania 1:8 — “Lakini kwa habari za Mwana asema,
‘kiti chako cha enzi, e Mungu, ni cha milele na
milele.” Tambua kwamba hapa Mungu Baba anamwita Yesu Mwana, “Mungu.” |
Waebrania 1:8 — “Lakini kumhusu Mwana: “Mungu ni
kiti chako cha ufalme milele na milele…” Mpangilio wa maneno umebadilishwa na shirika la Mashahidi wa Yehova ili kuficha ukweli kuwa Yesu (Mwana) anaitwa Mungu. |
Je, si ni hatari kufuata shirika linalobadilisha maandiko matakatifu.
3. MASHAHIDI WA YEHOVA WANA HISTORIA YA UNABII USIOTIMIZIKA
Viongozi wa Mashahidi wa Yehova wanadai kuzungumza kwa niaba ya Yehova Mungu kwa uwezo wa unabii lakini nyingi ya unabii wao ulishindwa kutimizika. Kwa mfano, walitabiri ya kuwa Armageddon na mwisho wa dunia ungelifanyika mwaka wa 1975. Kujaribu kuficha jambo hili, Mashahidi wa Yehova wengi hupinga ya kwamba hawakuwahi kutabiri hivi hata ingawa kuna dhibitisho katika vitabu vyao.1
Vile vile shirika la Mashahidi wa Yehova lilitabiri kuwa mwisho wa dunia ungelikuwako katika miaka ya 1914, 1915, 1918, 1925 na 1942. Walitabiri kuwa Ibrahimu, Isaka na Yakobo wangefufuka na warejee duniani mwaka wa 1925. Wametabiri mambo ya uongo kila wakati.2 Biblia inatangaza kuwa utabiri wa uongo ni kionyesho cha manabii wa uongo (Kumbukumbu 18:21-22).
Je, si ni hatari kufuata shirika ambalo lina historia ya utabiri usio wa kweli?
4. SHIRIKA LA MASHAHIDI WA YEHOVA HUTUMIA MAMLAKA YAKE VIBAYA
Licha ya utabiri wa uongo, shirika la Mashahidi wa Yehova linafunza kuwa dini yao pekee ndio ya kweli, na wafuasi wao pekee ndio wakristo kamili. Linadai kuwa hakuna anayeweza kujifunza ukweli wa kiroho isipokuwa wao. Pia linafunza kuwa kuna wokovu baada ya kujiunga tu na shirika lao na kuwa kila mtu, isipokuwa Mashahidi wa Yehova, atauawa kwenye Armageddon.
Shirika la Mashahidi wa Yehova linashurutisha wanachama wake kukubali, kutii na kuitikia bila kuuliza maswali, kila amri na maelezo ya Biblia ya shirika hilo. Kwa mfano shirika la Mashahidi wa Yehova linapinga vikali upaji damu (blood transfusion). Wafuasi wa shirika hili wanatarajiwa kibinafsi kufa au kuachilia watoto wao wafe badala ya kuvunja amri hii, hata ingawa Maandiko Matakatifu hayafunzi kuwa upaji damu ni vibaya. Mshahidi wa Yehova yeyote asiyetii amri hii anaambiwa kuwa atauawa katika Armageddon inayokuja – wakati wa hukumu ya mwisho.
Kupitia njia hii, viongozi wa shirika hili hutumia woga na kuwatisha wafuasi wao ili waendelee kutii shirika lao. Viongozi wa Mashahidi wa Yehova pia wametumia utabiri wa mwisho wa dunia ili kuwatisha wafuasi wao.
Je, si ni hatari kufuata shirika linalotumia mamlaka yake kwa njia mbaya?
Hoja hizi nne zinaonyesha hatari za kiroho zinazohusishwa na
shirika la Mashahidi wa Yehova. Pengine unashangaa, “Ni
habari gani njema ya Biblia?” Zifuatazo ni hoja nne
zinazoonyesha injili ya kweli ya Yesu Kristo kama
inavyopatikana katika Biblia.
Jinsi ya kuwa
na amani na Mungu
Ujumbe wa Biblia unaweza kufupishwa kwa
hoja nne rahisi:
1. Tumetenganishwa na Mungu wa kweli
na aishiye kwa sababu ya dhambi zetu.
“Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na
kupungukiwa na utukufu wa Mungu” Warumi 3:23.
“Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu
ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu” Warumi
6:23.
2. Hatuwezi tukajiokoa.
“Kwa hivyo hakuna mwenye mwili
atakayetangazwa kutakaswa mbele zake kwa matendo ya sheria;
kwa maana kufahamu dhambi huja kwa njia ya sheria” Warumi
3:20.
“Alituokoa sio kwa sababu ya wema
tulioufanya bali kwa sababu ya huruma yake.” Tito 3:5.
3. Yesu Kristo ndiye dawa
aliyoitumiya Mungu kwa tatizo la dhambi zetu.
“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda
ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila
amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” Yohana
3:16.
“Kwa maana Kristo naye alikufa mara moja
kwa ajili ya dhambi, aliyetakaswa kwa ajili yao
wasiotakaswa, ili awalete kwa Mungu” 1 Petero 3:18a.
4. Lazima tumpokee Yesu Kristo
kibinafsi kwa imani ili tupate kusamehewa dhambi na tupate
maisha ya milele.
“Bali kwa wale wote waliompokea, na
walioliamini jina lake, aliwapa uwezo kuwa watoto wa Mungu.”
Yohana 1:12
“… ukimkiri kwa kinywa chako kuwa ‘Yesu
ni Bwana,’ na uamini moyoni mwako kuwa Mungu alimfufua
katika wafu, utaokolewa”. Warumi 10:9.
Ikiwa ukweli huu kutoka kwa neno la Mungu umegusa moyo wako,
unaweza kukiri sasa hivi kwa kumuuliza akusamehe dhambi zako
na akupatie maisha mapya katika Kristo. Ombi hili rahisi
litakuongoza kuonyesha imani yako kwa Yesu Kristo kwa ajili
ya wokovu.
OMBI
Mwenyezi Mungu na mwenye huruma,
nakiri ya kwamba nimetenda dhambi mbele zako kwa vitendo,
maneno na fikira. Nimepungukiwa na wema na siwezi kujiokoa.
Ahsante sana kwa kumtuma mwanao Yesu Kristo kumwaga damu
yake kwa ajili yangu. Nakuomba unisamehe dhambi zangu zote,
na naweka imani yangu kwa Yesu Kristo aliyenifia na
akafufuka kutoka kwa wafu. Amina.
HOJA
1 The Watchtower, Agosti 15, 1968, uk. 499; Kingdom Ministry, Mai 1974, uk.3. Enda kwenye aya.
2 The Time is at Hand,
chapisho la 1906, uk. 99, 101; The
Time is at Hand, chapisho la 1915
uk. 99, 101; Pastor Russell’s Sermons,
chapisho la 1917 uk. 676; The
Finished Mystery, 1918, uk. 404,
485; The Watchtower, Septemba 1,
1922 uk. 262; The Watchtower,
Septemba 15, 1941 uk. 288; Millions
Now Living Will Never Die, 1920, uk.
88-90. Enda kwenye aya.

